Viongozi wa kandaa waipongeza Kenya kwa hatua ilizoafikia katika Reli ya Kisasa ya SGR, huku wakiyahimiza mataifa mengine kuiga mfano huo

NAIROBI, 26 JUNI 2018 (PSCU) — Viongozi wa kandaa hii wameipongeza Kenya kwa  hatua  ilizoafikia katika ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR, ambao sasa wanazitaka Uganda, Rwanda na Sudan Kusini kuiga mfano huo.

Viongozi hao  ambao walihudhuria  mkutano wao wa 14 kuhusu miradi ya ushirikishi ya ushoroba wa kaskazini hasa waliridhishwa na  kujitolea kwa Kenya katika kutekeleza mradi wa reli ya kisasa huku ikiwa imekamilisha awamu ya kwanza ya reli hiyo kutoka Mombasa hadi Nairobi na kuchukua hatua nyingine zaidi ya kuanzisha awamu ya pili ya kutoka Nairobi hadi Naivasha.

“Mkutano huu wa viongozi ulisifu uzinduzi na ukamilifu wa awamu ya kutoka Mombasa-Nairobi mnamo mwaka wa 2017 ambayo sasa inasafirisha kwa wingi abiria na mizigo,” viongozi hao walisema katika taarifa yao ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano huo uliofanyika Nairobi.

Mkutano huo ambao uliandaliwa na Rais Uhuru Kenyatta, ulihudhuriwa na  Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Rais  Paul Kagame wa Rwanda huku Rais Salva Kiiri wa Sudan Kusini akiwakilishwa na mjumbe maalumu Bw.Aggrey Tisa Sabuni.

Akizunguza baada ya kumalizika kwa mkutano huo, Rais Kenyatta alisisitiza manufaa ya  miradi ya pamoja inayoanzishwa chini ya  Miradi ya Ushirikishi wa Ushoroba wa Kazkazini tangu kunzishwa kwake mnamo mwaka wa 2013.

“Bila shaka hii ni habari njema kwa raia wetu,” alisema Rais huku akitoa mfano wa hatua za pamoja ikiwemo kuwepo kwa eneo moja la utozaji ushuru ambalo limesaidia katika kupunguza muda  na gharama ya uchukuzi wa mizigo ya kusafirishwa nchi jirani.

Vile vile, Rais Kenyatta aliwahakikishia wenzake kwamba Kenya  itadumisha kasi ya kutekeleza na kukamilisha  awamu zilizosalia za mradi wa SGR kufika katika mji wa  Malaba ulioko katika  mpaka kati ya Kenya na Uganda .

Kwa upande wake, Rais Museveni alisema yeye hufurahia kila anapohudhuria mkutano huo  kwani uchumi wa Uganda unategemea sana nchi jirani zikiongozwa na Kenya ambayo hununua kiasi kikubwa cha mazao yake ya mahindi na maziwa.

Rais Museveni aliwahimiza maafisa wa Halmashauri ya Ushuru ya Uganda walioko katika bandari ya Mombasa kufanya kazi kwa masaa zaidi kama wenzao wa Kenya kuhakikisha hakuna msongamano wa mizigo inayokusudiwa kusafirishwa nchini Uganda.

Rais Kagame alimshukuru Rais Kenyatta kwa kuandaa mkutano huo wa viongozi baada ya mapumziko ya miaka miwili.

“Namshukuru sana Rais Kenyatta kwa kuandaa tena mkutano huu baada ya kipindi cha karibu miaka miwili ili tuweze kuendelea na kasi ya kuratibu na kutekeleza miradi ya pamoja kwa manufaa ya eneo hili,” akasema Rais Kagame.

Kwenye taarifa ya pamoja, viongozi hao wa Afrika Mashariki walikariri kujitolea kwao kuendeleza ushirikishi wa eneo hili huku wakisisitiza umuhimu wa kuharakisha mabadidiliko ya kijamii na kiuchumi, ujenzi wa viwanda na ubunifu wa ajira.

Ili kurahisisha usambazaji wa bidhaa za mafuta katika eneo hili hii ikiwa ni chanzo cha viwanda na kawi, viongozi hao walikubaliana kubuni mfumo wa uchukuzi wa pamoja huku wakisuburi kushauriana  zaidi kuhusu masuala ya bidhaa zilizotayarishwa za mafuta ya petroli pamoja na bomba la mafuta hayo.

Vile vile, viongozi hao walikubaliana kutenga fedha zaidi kwa ustawi wa vituo vya ubora zaidi ili kuunga mkono uthibiti wa wafanyakazi wenye ujuzi ambao wanahitajika kwa utekelezaji na udumishaji wa miradi ya ushirikishi wa  ushoroba wa kaskkazini (NCIP).

Kuhusu kuanzishwa kwa kituo cha ubadilishaji bidhaa, mkutano huo alipashwa habari kuhusu ushirikishi wa viwango vinavyotumika kwa biashara ya bidhaa za eneo hili na wakaagiza mataifa wanachama kuharakisha utaratibu unaohitajika.

“Mkutano huu unaagiza mataifa wanachama kuharakisha ustawi wa majukwaa ya kibiashara,” Viongozi hao walisema kwenye taarifa yao ya pamoja.

Mkutano huo ulijadilia na kuamua kukubali Mkataba wa Ulinzi huku wakikubaliana kuhusu  kubuniwa kwa  Kituo cha Tarakimu za uchukuzi wa ndege kwa ajili ya Ushoroba huo wa Kaskazini.

Viongozi hao pia walijadilia kuhusu shughuli katika bandari ya Mombasa, kituo cha kuingilia na kusafirisha mizigo huku wakiagiza mashirika husika kuhakikisha uadilifu na usawa katika shughuli za kupitisha mizigo.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Naibu Rais wa Kenya William Ruto na vile vile wawakilishi kutoka Tanzania, Burundi na Ethiopia, yakiwa ni mataifa yenye fursa ya kufanya uchunguzi katika mkutano huo wa NCIP.